Mwanzo 1:1-9
Mwanzo 1:1-9 NEN
Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji. Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza. Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo.