Mwanzo 12:1-9
Mwanzo 12:1-9 NENO
Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Abramu, “Ondoka katika nchi yako, uache jamii yako na nyumba ya baba yako, uende hadi nchi nitakayokuonesha. “Nitakufanya taifa kubwa na nitakubariki, Nitalikuza jina lako, nawe utakuwa baraka. Nitawabariki wale wanaokubariki, na yeyote akulaaniye nitamlaani; na kupitia kwako mataifa yote duniani yatabarikiwa.” Hivyo Abramu akaondoka kama Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwambia; naye Lutu akaondoka pamoja naye. Abramu alipoitwa aondoke Harani, alikuwa na umri wa miaka sabini na tano. Abramu akamchukua Sarai mkewe pamoja na Lutu mwana wa ndugu yake, mali yote waliyokuwa nayo, pamoja na watu aliokuwa amewapata huko Harani, wakasafiri kwenda nchi ya Kanaani, na wakafika huko. Abramu akasafiri katika nchi hiyo hadi huko Shekemu, mahali penye mwaloni wa More. Wakati huo Wakanaani walikuwa wanaishi katika nchi hiyo. Mwenyezi Mungu akamtokea Abramu, akamwambia, “Nitawapa uzao wako nchi hii.” Hivyo hapo akamjengea madhabahu Mwenyezi Mungu aliyekuwa amemtokea. Kutoka huko Abramu akasafiri kuelekea kwenye vilima mashariki mwa Betheli, naye akapiga hema huko, Betheli ikiwa upande wa magharibi na Ai upande wa mashariki. Huko alimjengea Mwenyezi Mungu madhabahu na akaliitia jina la Mwenyezi Mungu. Kisha Abramu akasafiri kuelekea upande wa Negebu.