Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 14:1-16

Mwanzo 14:1-16 NENO

Wakati huo Amrafeli mfalme wa Shinari, Arioko mfalme wa Elasari, Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu walienda kupigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari). Wafalme wa kundi hili la pili waliunganisha majeshi yao katika Bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi). Walikuwa wametawaliwa na Mfalme Kedorlaoma kwa miaka kumi na mbili, lakini mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Mwaka wa kumi na nne, Mfalme Kedorlaoma na wafalme waliojiunga naye walienda vitani na wakawashinda Warefai katika Ashtaroth-Kanaimu, Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe-Kiriathaimu, na Wahori katika nchi ya vilima ya Seiri, hadi El-Parani karibu na jangwa. Kisha wakarudi, wakaenda En-Misfati (yaani Kadeshi), wakashinda nchi yote ya Waamaleki, pamoja na Waamori walioishi Hasason-Tamari. Ndipo mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari) wakatoka kupanga majeshi yao kwenye Bonde la Sidimu dhidi ya Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari; yaani wafalme wanne dhidi ya wafalme watano. Basi Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, nao wafalme wa Sodoma na wa Gomora walipokimbia, baadhi ya watu walitumbukia huko na wengine wakakimbilia vilimani. Wale wafalme wanne wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora pamoja na vyakula vyao vyote, kisha wakaenda zao. Pia walimteka Lutu, mwana wa ndugu yake Abramu, pamoja na mali yake, kwa kuwa alikuwa akiishi Sodoma. Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, ndugu ya Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu. Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu mia tatu na kumi na nane (318) wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani. Wakati wa usiku, Abramu aliwapanga watu wake katika vikosi, wakawashambulia na kuwashinda, wakawafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Dameski. Abramu akarudisha mali yote, na akamrudisha Lutu jamaa yake na mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.