Mwanzo 14:1-16
Mwanzo 14:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, mfalme Amrafeli wa Shinari, mfalme Arioko wa Elasari, mfalme Kedorlaomeri wa Elamu na mfalme Tidali wa Goiimu, walipigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, dhidi ya Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na dhidi ya mfalme wa Bela (yaani Soari). Wafalme hao watano waliyaunganisha majeshi yao katika bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi). Kwa muda wa miaka kumi na miwili walikuwa wakimtii mfalme Kedorlaomeri, lakini mnamo mwaka wa kumi na tatu, walimwasi. Mnamo mwaka wa kumi na nne, mfalme Kedorlaomeri na wale wafalme wenzake walikuja na kuwashinda watu wa Refaimu huko Ashtaroth-karnaimu, na Wazuzi huko Hamu, na Waemi huko Shawe-kiriathaimu, na Wahori huko mlimani kwao Seiri, wakawafukuza hadi Elparani, mpakani mwa jangwa. Kisha wakarudi nyuma mpaka Enmishpati (yaani Kadeshi), wakaivamia nchi yote ya Waamaleki, na kuwashinda Waamori waliokaa Hasason-tamari. Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu na mfalme wa Bela (yaani Soari), wakaingia vitani katika bonde la Sidimu kupigana na Kedorlaomeri mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goiimu, Amrafeli mfalme wa Shinari na Arioko mfalme wa Elasari; wafalme wanne dhidi ya wafalme watano. Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami; kwa hiyo wafalme wa Sodoma na Gomora walipokuwa wakiikimbia vita, wakatumbukia humo, lakini wengine wakatorokea mlimani. Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao. Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu. Abramu alipopata habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka, akatoka na watu wake stadi 318 waliozaliwa katika nyumba yake, akawafuatia adui mpaka Dani. Huko, akaligawa jeshi lake katika makundi. Usiku, akawashambulia adui zake, akawashinda na kuwafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Damasko. Basi, Abramu akaikomboa mali yote iliyotekwa na adui, na kumkomboa Loti mpwa wake, mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.
Mwanzo 14:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari. Hawa wote wakakutana katika bonde la Sidimu, yaani Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu, na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; aliyekuwa akikaa karibu na mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye amechukuliwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.
Mwanzo 14:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari. Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu, na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.
Mwanzo 14:1-16 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Wakati huo Amrafeli mfalme wa Shinari, Arioko mfalme wa Elasari, Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu walienda kupigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari). Wafalme wa kundi hili la pili waliunganisha majeshi yao katika Bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi). Walikuwa wametawaliwa na Mfalme Kedorlaoma kwa miaka kumi na mbili, lakini mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Mwaka wa kumi na nne, Mfalme Kedorlaoma na wafalme waliojiunga naye walienda vitani na wakawashinda Warefai katika Ashtaroth-Kanaimu, Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe-Kiriathaimu, na Wahori katika nchi ya vilima ya Seiri, hadi El-Parani karibu na jangwa. Kisha wakarudi, wakaenda En-Misfati (yaani Kadeshi), wakashinda nchi yote ya Waamaleki, pamoja na Waamori walioishi Hasason-Tamari. Ndipo mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari) wakatoka kupanga majeshi yao kwenye Bonde la Sidimu dhidi ya Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari; yaani wafalme wanne dhidi ya wafalme watano. Basi Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, nao wafalme wa Sodoma na wa Gomora walipokimbia, baadhi ya watu walitumbukia huko na wengine wakakimbilia vilimani. Wale wafalme wanne wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora pamoja na vyakula vyao vyote, kisha wakaenda zao. Pia walimteka Lutu, mwana wa ndugu yake Abramu, pamoja na mali yake, kwa kuwa alikuwa akiishi Sodoma. Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, ndugu ya Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu. Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu mia tatu na kumi na nane (318) wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani. Wakati wa usiku, Abramu aliwapanga watu wake katika vikosi, wakawashambulia na kuwashinda, wakawafukuza hadi Hoba, kaskazini mwa Dameski. Abramu akarudisha mali yote, na akamrudisha Lutu jamaa yake na mali yake, pamoja na wanawake na watu wengine.