Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 38:1-11

Mwanzo 38:1-11 NENO

Wakati ule, Yuda akawaacha ndugu zake, akaenda kuishi na Hira Mwadulami. Huko Yuda akakutana na binti ya Mkanaani aitwaye Shua. Akamwoa na akakutana naye kimwili, naye akapata mimba, na akamzaa mwana, aliyeitwa jina Eri. Akapata mimba tena, akamzaa mwana na kumwita jina Onani. Akamzaa mwana mwingine tena, akamwita jina Shela. Huyu alimzalia huko Kezibu. Yuda akamtwalia Eri, mzaliwa wake wa kwanza, mke aliyeitwa Tamari. Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mwovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akamuua. Kisha Yuda akamwambia Onani, “Kutana kimwili na mke wa ndugu yako, na utimize wajibu wako kwake kama mke wa ndugu yako, ili umpatie ndugu yako uzao.” Lakini Onani alijua kwamba uzao haungekuwa wake, kwa hiyo kila alipokutana kimwili na mke wa ndugu yake, alimwaga mbegu chini ili asimpatie ndugu yake uzao. Alichofanya kilikuwa kiovu machoni pa Mwenyezi Mungu, hivyo Mwenyezi Mungu akamuua Onani pia. Kisha Yuda akamwambia Tamari mkwewe, “Ishi kama mjane nyumbani mwa baba yako hadi mwanangu Shela atakapokua.” Kwa maana alifikiri, “Anaweza kufa pia kama ndugu zake.” Kwa hiyo Tamari akaenda kuishi nyumbani mwa baba yake.