Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 45:16-28

Mwanzo 45:16-28 NENO

Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yusufu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. Farao akamwambia Yusufu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi hadi nchi ya Kanaani, mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri, nanyi mtafurahia unono wa nchi.’ “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. Msijali kamwe kuhusu mali yenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ” Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yusufu akawapa magari ya kukokotwa kama Farao alivyoagiza, na pia akawapa chakula cha safari yao. Akampa kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli mia tatu za fedha, na jozi tano za nguo. Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliobeba vitu vizuri vya Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!” Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. Wakamwambia baba yao, “Yusufu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki. Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yusufu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yusufu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yusufu bado yu hai. Nitaenda nikamwone kabla sijafa.”