Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 45

45
Yusufu ajitambulisha
1Basi Yusufu hakuweza kujizuia tena mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye. Akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwa mtu mwingine na Yusufu alipojitambulisha kwa ndugu zake. 2Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.
3Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yusufu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.
4Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yusufu, yule ambaye mlimuuza Misri! 5Sasa msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. 6Kwa miaka miwili sasa njaa imekuwa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwa na kulima wala kuvuna. 7Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.
8“Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kama baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote. 9Sasa rudini haraka kwa baba yangu, mkamwambie, ‘Hili ndilo mwanao Yusufu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa mtawala wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie. 10Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami: wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na vyote ulivyo navyo. 11Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulio nao mtakuwa fukara.’
12“Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi. 13Mwambieni baba yangu kuhusu heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”
14Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia. 15Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo, ndugu zake wakazungumza naye.
16Habari zilipofika kwenye jumba la Farao kwamba ndugu zake Yusufu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi. 17Farao akamwambia Yusufu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi hadi nchi ya Kanaani, 18mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri, nanyi mtafurahia unono wa nchi.’
19“Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. 20Msijali kamwe kuhusu mali yenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ”
21Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yusufu akawapa magari ya kukokotwa kama Farao alivyoagiza, na pia akawapa chakula cha safari yao. 22Akampa kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli mia tatu#45:22 Shekeli 300 za fedha ni sawa na kilo 3.4. za fedha, na jozi tano za nguo. 23Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliobeba vitu vizuri vya Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari. 24Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”
25Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani. 26Wakamwambia baba yao, “Yusufu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuazi; hakuwasadiki. 27Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yusufu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yusufu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa. 28Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yusufu bado yu hai. Nitaenda nikamwone kabla sijafa.”

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 45: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia