Mwanzo 44
44
Kikombe cha fedha ndani ya gunia
1Kisha Yusufu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu katika gunia lake. 2Kisha weka kikombe changu kile cha fedha katika gunia la yule mdogo wa wote, pamoja na fedha zake ambazo alinunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yusufu alivyosema.
3Kulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda wao. 4Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yusufu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja; utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya? 5Je, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu, na pia hukitumia kwa kubashiri? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’ ”
6Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao. 7Lakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako kufanya jambo kama hilo! 8Tazama, tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye magunia yetu. Hivyo, kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani mwa bwana wako? 9Ikiwa yeyote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”
10Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Yeyote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”
11Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua. 12Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini. 13Kwa hilo, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda wao na kurudi mjini.
14Yusufu alikuwa bado yuko nyumbani mwake Yuda na ndugu zake walipoingia. Wote wakajitupa chini mbele yake. 15Yusufu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kubashiri?”
16Yuda akajibu, “Tuseme nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”
17Lakini Yusufu akasema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine rudini kwa baba yenu kwa amani.”
18Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe. 19Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’ 20Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’
21“Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’ 22Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’ 23Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’ 24Tuliporudi kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.
25“Ndipo baba yetu alisema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’ 26Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri hadi ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutaenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu hadi ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’
27“Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili. 28Mmoja alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo. 29Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’
30“Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu, 31akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni. 32Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sitamrudisha kwako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’
33“Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi wako abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake. 34Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 44: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.