Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 43

43
Safari ya pili kwenda Misri
1Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi. 2Hivyo wakati walikuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine.”
3Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena hadi mje na ndugu yenu.’ 4Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutaenda kuwanunulia chakula. 5Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutaenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena hadi mje na ndugu yenu.’ ”
6Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?”
7Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado angali hai? Je, mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo yenu hapa’?”
8Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara moja, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife. 9Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake; mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Nisipomrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote. 10Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumeenda na kurudi mara mbili.”
11Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni sehemu ya bidhaa bora za nchi katika mifuko yenu, na mmpelekee yule mtu kama zawadi: zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi. 12Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa. 13Mchukueni ndugu yenu pia, mrudi kwa huyo mtu mara moja. 14Naye Mungu Mwenyezi#43:14 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote). awajalie rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi, kama nikufiwa, nimefiwa.”
15Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na wakajionesha kwa Yusufu. 16Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani mwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula, kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”
17Msimamizi akafanya kama Yusufu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani mwa Yusufu. 18Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani mwa Yusufu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda wetu.”
19Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yusufu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumba. 20Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula. 21Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake katika gunia lake, kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha. 22Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.”
23Akawaambia, “Vema, msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.
24Msimamizi akawapeleka wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji ya kunawa miguu, na kuwapa punda wao majani. 25Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yusufu atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko.
26Yusufu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia. 27Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?”
28Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama, wakamsujudia.
29Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.” 30Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yusufu akaondoka kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo.
31Baada ya kunawa uso wake, akarudi; huku akijizuia kulia, akasema, “Pakueni chakula.”
32Wakampakulia Yusufu peke yake, nao ndugu zake peke yao, na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri. 33Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao. 34Walipopelekewa sehemu ya chakula kutoka meza ya Yusufu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 43: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia