Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Habakuki 2

2
1Nitasimama katika zamu yangu,
na kujiweka juu ya maboma;
nitatazama nione atakaloniambia,
na jibu nitakalotoa kuhusu lalamiko hili.
Jibu la Mwenyezi Mungu
2Kisha Mwenyezi Mungu akajibu:
“Andika ufunuo huu,
na ukaufanye wazi juu ya vibao,
ili mpiga mbiu akimbie nao.
3Kwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika;
unazungumzia mambo ya mwisho,
na kamwe hautakosea.
Iwapo utakawia, wewe usubiri;
kwa hakika utakuja na hautachelewa.
4“Tazama, amejaa majivuno;
anavyovitamani si vya unyofu:
lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake:
5hakika mvinyo humsaliti;
ni mwenye kiburi na hana amani.
Kwa sababu ni mlafi kama Kuzimu#2:5 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho.,
na kama kifo kamwe hatosheki;
anajikusanyia mataifa yote
na kuchukua watu wote mateka.
6“Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema,
“ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa
na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu!
Ataendelea hivi kwa muda gani?’
7Je, wadai wako hawatainuka ghafula?
Je, hawataamka na kukufanya utetemeke?
Kisha utakuwa mhanga kwao.
8Kwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi,
watu waliobaki watakuteka nyara wewe.
Kwa kuwa umemwaga damu ya watu;
umeharibu nchi na miji, na watu wote wanaoishi humo.
9“Ole wake yeye ajengaye milki yake kwa mapato ya udhalimu,
awekaye kiota chake juu,
ili kukimbia makucha ya uharibifu!
10Umepanga njama ya maangamizi ya watu wengi,
ukiaibisha nyumba yako mwenyewe,
na kupotewa na maisha yako.
11Mawe ya kuta yatapiga kelele,
na mihimili ya kazi ya mbao itarudisha mwangwi wake.
12“Ole wake yeye ajengaye mji kwa kumwaga
damu na kuusimamisha mji kwa uhalifu!
13Je, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni hakuonesha
kwamba kazi ya wanadamu ni mafuta tu kwa ajili ya moto,
na kwamba mataifa
yanajichosha bure?
14Kwa kuwa dunia itajazwa na maarifa ya utukufu wa Mwenyezi Mungu,
kama maji yaifunikavyo bahari.
15“Ole wake yeye awapaye majirani zake kileo,
akikimimina kutoka kwa kiriba cha mvinyo hadi wamelewa,
ili apate kutazama miili yao iliyo uchi.
16Utajazwa na aibu badala ya utukufu.
Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue!
Kikombe kutoka mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu kinakujia,
na aibu itafunika utukufu wako.
17Ukatili ulioifanyia Lebanoni utakufunika,
na uharibifu uliowafanyia wanyama utakutisha.
Kwa sababu umemwaga damu ya mtu;
umeharibu nchi na miji na kila mmoja aliye ndani yake.
18“Sanamu ina thamani gani,
kwani mwanadamu ndiye alichonga?
Ama kinyago kinachofundisha uongo?
Kwa kuwa yeye aliyekitengeneza
hutegemea kazi ya mikono yake mwenyewe;
hutengeneza sanamu zisizoweza kuzungumza.
19Ole wake yeye auambiaye mti, ‘Uwe hai!’
Ama asemaye na jiwe lisilo na uhai, ‘Amka!’
Je, linaweza kuongoza?
Limefunikwa kwa dhahabu na fedha;
hakuna pumzi ndani yake.
20Lakini Mwenyezi Mungu yuko katika Hekalu lake takatifu;
dunia yote na inyamaze mbele yake.”

Iliyochaguliwa sasa

Habakuki 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia