Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 2

2
1“Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’
Israeli kuadhibiwa na kurudishwa
2“Mkemeeni mama yenu, mkemeeni,
kwa maana yeye si mke wangu,
nami si mume wake.
Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake
na uzinzi kati ya matiti yake.
3Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi
na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa.
Nitamfanya kama jangwa,
nitamgeuza awe nchi ya kiu,
nami nitamuua kwa kiu.
4Sitaonesha upendo wangu kwa watoto wake,
kwa sababu ni watoto wa uzinzi.
5Mama yao amekosa uaminifu
na amewachukua mimba katika aibu.
Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu,
ambao hunipa chakula changu
na maji yangu,
sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu
na kinywaji changu.’
6Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake
kwa vichaka vya miiba,
nitamjengea ukuta ili
asiweze kutoka.
7Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata;
atawatafuta lakini hatawapata.
Kisha atasema,
‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza,
kwa maana nilikuwa na hali njema
kuliko sasa.’
8Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye
niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta,
niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia
kwa kumtumikia Baali.
9“Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa
na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari.
Nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu
iliyokusudiwa kufunika uchi wake.
10Basi sasa nitaufunua ufisadi wake
mbele ya wapenzi wake;
hakuna yeyote atakayemtoa
mikononi mwangu.
11Nitakomesha furaha na macheko yake yote:
sikukuu zake za mwaka,
sikukuu za Miandamo ya Mwezi,
siku zake za Sabato,
sikukuu zake zote zilizoamriwa.
12Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake,
ambayo alisema yalikuwa malipo yake
kutoka kwa wapenzi wake;
nitaifanya kuwa kichaka,
nao wanyama pori wataila.
13Nitamwadhibu kwa ajili ya siku
alizowafukizia uvumba Mabaali;
alipojipamba kwa pete
na kwa vito vya thamani,
na kuwaendea wapenzi wake,
lakini mimi alinisahau,”
asema Mwenyezi Mungu.
14“Kwa hiyo sasa nitamshawishi;
nitamwongoza hadi jangwani
na kuzungumza naye kwa upole.
15Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu,
nami nitalifanya Bonde la Akori#2:15 yaani Bonde la Taabu
mlango wa matumaini.
Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake,
kama siku zile alizotoka Misri.
16“Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu,
“utaniita mimi ‘Mume wangu#2:16 Mume wangu Kiebrania ni Ishi’;
hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu#2:16 Bwana wangu Kiebrania ni Baal.’
17Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka mdomoni mwake,
wala hataomba tena kwa majina yao.
18Katika siku ile nitafanya agano kwa ajili yao
na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani,
na viumbe vinavyotambaa ardhini.
Upinde, upanga na vita,
nitaondolea mbali katika nchi,
ili wote waweze kukaa salama.
19Nitakuposa uwe wangu milele;
nitakuposa kwa uadilifu na haki,
kwa upendo na huruma.
20Nitakuposa kwa uaminifu,
nawe utamkubali Mwenyezi Mungu.
21“Katika siku ile nitajibu,”
asema Mwenyezi Mungu,
“nitajibu kwa anga,
nazo anga zitajibu kwa nchi;
22nayo nchi itajibu kwa nafaka,
divai mpya na mafuta,
navyo vitajibu kwa Yezreeli.
23Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe;
nami nitaonesha pendo langu kwake
yule ambaye nilimwita, ‘Si Mpendwa Wangu#2:23 Kiebrania ni Lo-Ruhama (taz. 1:6)..’
Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio Watu Wangu#2:23 Kiebrania ni Lo-Ami (taz. 1:9).,’
‘Ninyi ni Watu Wangu’;
nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu’.”

Iliyochaguliwa sasa

Hosea 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia