4
Shtaka dhidi ya Israeli
1Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi Waisraeli,
kwa sababu Mwenyezi Mungu analo shtaka
dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:
“Hakuna uaminifu, hakuna upendo,
hakuna kumjua Mungu katika nchi.
2Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,
wizi na uzinzi,
bila kuwa na mipaka,
nao umwagaji damu mmoja
baada ya mwingine.
3Kwa sababu hii nchi huomboleza,
wote wanaoishi ndani yake wanadhoofika;
wanyama wa kondeni, ndege wa angani
na samaki wa baharini wanakufa.
4“Lakini mtu yeyote na asilete shtaka,
mtu yeyote na asimlaumu mwenzake,
kwa maana watu wako ni kama wale
waletao mashtaka dhidi ya kuhani.
5Unajikwaa usiku na mchana,
nao manabii hujikwaa pamoja nawe.
Kwa hiyo nitamwangamiza mama yako:
6watu wangu wanaangamizwa
kwa kukosa maarifa.
“Kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa,
mimi nami nitakukataa wewe
usiwe kuhani kwangu mimi;
kwa kuwa umeacha kuijali Torati ya Mungu wako
mimi nami sitawajali watoto wako.
7Kadiri makuhani walivyoongezeka,
ndivyo walivyozidi kutenda dhambi dhidi yangu,
walibadilisha utukufu wao kwa kitu cha aibu.
8Wanajilisha dhambi za watu wangu
na kupendezwa na uovu wao.
9Hata itakuwa: Kama walivyo watu,
ndivyo walivyo makuhani.
Nitawaadhibu wote wawili kwa ajili ya njia zao
na kuwalipa kwa matendo yao.
10“Watakula lakini hawatashiba;
watajiingiza katika ukahaba
lakini hawataongezeka,
kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu
na kujiingiza wenyewe
11katika ukahaba;
kunywa divai ya zamani na divai mpya
huondoa ufahamu
12wa watu wangu.
Hutaka shauri kutoka kwa sanamu ya mti
nao hujibiwa na fimbo ya mti.
Roho ya ukahaba imewapotosha,
hawana uaminifu kwa Mungu wao.
13Wanatoa dhabihu juu ya vilele vya milima
na sadaka za kuteketezwa juu ya vilima,
chini ya mialoni, milibua na miela,
ambako kuna vivuli vizuri.
Kwa hiyo binti zenu wamegeukia ukahaba
na wake za wana wenu uzinzi.
14“Sitawaadhibu binti zenu wakati
wanapogeukia ukahaba,
wala wake za wana wenu
wanapofanya uzinzi,
kwa sababu wanaume wenyewe huandamana na malaya
na kutambikia pamoja na makahaba
wa mahali pa ibada za sanamu:
watu wasiokuwa na ufahamu
wataangamia!
15“Ingawa umefanya uzinzi, ee Israeli,
Yuda naye asije akawa na hatia.
“Usiende Gilgali,
usipande kwenda Beth-Aveni#4:15 maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu); yaani Betheli kwa dhihaka.
Wala usiape,
‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo!’
16Waisraeli ni wakaidi,
kama ndama jike mkaidi.
Ni jinsi gani basi Mwenyezi Mungu anaweza kuwachunga
kama wana-kondoo
katika shamba la majani?
17Efraimu amejiunga na sanamu,
achana naye!
18Hata wakati wamemaliza vileo vyao
wanaendelea na ukahaba wao,
watawala wao hupenda sana
njia za aibu.
19Kisulisuli kitawafagilia mbali
na dhabihu zao zitawaletea aibu.