Isaya 19:16-25
Isaya 19:16-25 NENO
Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa BWANA wa majeshi anaoinua dhidi yao. Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho BWANA wa majeshi anapanga dhidi yao. Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii BWANA wa majeshi. Mji mmoja utaitwa Mji wa Uharibifu. Katika siku hiyo patakuwa na madhabahu ya BWANA katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa BWANA kwenye mpaka wa Misri. Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya BWANA wa majeshi katika nchi ya Misri. Watakapomlilia BWANA kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa. Hivyo BWANA atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali BWANA. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea BWANA nadhiri na kuzitimiza. BWANA ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia BWANA, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya. Katika siku hiyo kutakuwa na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru wataenda Misri, na Wamisri wataenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja. Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia. BWANA wa majeshi atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”