Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 38

38
Ugonjwa wa Hezekia
(2 Wafalme 20:1-11; 2 Nyakati 32:24-26)
1Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
2Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Mwenyezi Mungu: 3“Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
4Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Isaya, kusema: 5“Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako. 6Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.
7“ ‘Hii ndiyo ishara ya Mwenyezi Mungu kwako kwamba Mwenyezi Mungu atafanya kile alichoahidi: 8Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.
9Maandiko ya Hezekia mfalme wa Yuda baada ya kuugua kwake na kupona:
10Nilisema, “Katika ustawi wa maisha yangu,
je, ni lazima nipite katika malango ya mauti#38:10 yaani Kuzimu,
na kupokonywa miaka yangu iliyobaki?”
11Nilisema, “Sitamwona tena Mwenyezi Mungu,
Mwenyezi Mungu katika nchi ya walio hai,
wala sitamtazama tena mwanadamu,
wala kuwa na wale ambao sasa wanakaa katika ulimwengu huu.
12Kama hema la mchunga mifugo,
nyumba yangu imebomolewa na kutwaliwa kutoka kwangu.
Kama mfumaji nimevingirisha maisha yangu,
naye amenikatilia mbali kutoka kitanda cha mfumi.
Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
13Nilingoja kwa uvumilivu hadi mapambazuko,
lakini alivunja mifupa yangu yote kama simba.
Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
14Nililia kama mbayuwayu au korongo,
niliomboleza kama hua aombolezaye.
Macho yangu yalififia nilipotazama mbinguni.
Ee Bwana, ninataabika, njoo unisaidie!”
15Lakini niseme nini?
Amesema nami, naye yeye mwenyewe amelitenda hili.
Nitatembea kwa unyenyekevu
katika miaka yangu yote
kwa sababu ya haya maumivu makali
ya nafsi yangu.
16Bwana, kwa mambo kama haya watu huishi,
nayo roho yangu hupata uzima katika hayo pia.
Uliniponya
na kuniacha niishi.
17Hakika ilikuwa ya faida yangu
ndiyo maana nikapata maumivu makali.
Katika upendo wako ukaniokoa
kutoka shimo la uharibifu;
umeziweka dhambi zangu zote
nyuma yako.
18Kwa maana kaburi#38:18 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu; kwa Kiebrania ni Sheol. haliwezi kukusifu,
mauti haiwezi kuimba sifa zako;
wale wanaoshuka shimoni
hawawezi kuutarajia uaminifu wako.
19Walio hai, walio hai: hao wanakusifu,
kama ninavyofanya leo.
Baba huwaambia watoto wao
habari za uaminifu wako.
20Mwenyezi Mungu ataniokoa,
nasi tutaimba kwa vyombo vya nyuzi
siku zote za maisha yetu
katika Hekalu la Mwenyezi Mungu.
21Isaya alikuwa amesema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini, mweke juu ya jipu, naye atapona.”
22Hezekia alikuwa ameuliza, “Kutakuwa na ishara gani kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Mwenyezi Mungu?”

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 38: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia