Isaya 40
40
Faraja kwa watu wa Mwenyezi Mungu
1Wafarijini, wafarijini watu wangu,
asema Mungu wenu.
2Sema na Yerusalemu kwa upole,
umtangazie
kwamba kazi yake ngumu imekamilika,
kwamba dhambi yake imelipiwa fidia,
kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Mwenyezi Mungu
maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.
3Sauti ya mtu aliaye nyikani:
“Itengenezeni njia ya Mwenyezi Mungu jangwani,
yanyoosheni mapito nyikani
kwa ajili ya Mungu wetu.
4Kila bonde litainuliwa,
kila mlima na kilima kitashushwa;
penye mabonde patanyooshwa,
napo palipoparuza patasawazishwa.
5Utukufu wa Mwenyezi Mungu utafunuliwa,
nao wanadamu wote watauona pamoja.
Kwa maana kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena.”
6Sauti husema, “Piga kelele.”
Nami nikasema, “Nipige kelele gani?”
“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao wote
ni kama maua ya kondeni.
7Majani hunyauka na maua huanguka,
kwa sababu pumzi ya Mwenyezi Mungu huyapuliza.
Hakika wanadamu ni majani.
8Majani hunyauka na maua huanguka,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
9Wewe uletaye habari njema Sayuni,
panda juu ya mlima mrefu.
Wewe uletaye habari njema Yerusalemu,
paza sauti yako, piga kelele kwa nguvu,
paza sauti, usiogope;
iambie miji ya Yuda,
“Yuko hapa Mungu wenu!”
10Tazameni, Bwana Mungu Mwenyezi anakuja na nguvu,
nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake.
Tazameni, ujira wake u pamoja naye,
nayo malipo yake yanafuatana naye.
11Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo:
Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake
na kuwachukua karibu na moyo wake,
huwaongoza taratibu wale wanaonyonyesha.
12Ni nani aliyepima maji ya bahari
kwenye konzi ya mkono wake,
au kuzipima mbingu kwa shibiri yake?
Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu,
au kupima milima kwenye kipimio
na vilima kwenye mizani?
13Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Mwenyezi Mungu,
au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?
14Ni nani ambaye Mwenyezi Mungu ametaka shauri kwake ili kumwelimisha,
naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa?
Ni nani aliyemfundisha maarifa
au kumwonesha mapito ya ufahamu?
15Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo,
ni kama vumbi jembamba juu ya mizani,
huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.
16Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni,
wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa.
17Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu,
yanaonekana yasio na thamani
na zaidi ya bure kabisa.
18Basi, utamlinganisha Mungu na nani?
Utamlinganisha na kitu gani?
19Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu,
naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu
na kuitengenezea mikufu ya fedha.
20Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii
huuchagua mti usiooza.
Humtafuta fundi stadi
wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika.
21Je, hujui?
Je, hujasikia?
Je, hujaambiwa tangu mwanzo?
Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia?
22Anakaa kwenye kiti cha utawala juu ya duara ya dunia,
nao watu wanaoishi humo ni kama panzi.
Huzitandaza mbingu kama chandarua,
na kuzitandaza kama hema la kuishi.
23Huwafanya wakuu kuwa si kitu,
na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure.
24Mara baada ya kupandwa,
mara baada ya kutiwa ardhini,
mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini,
ndipo huwapulizia nao wakanyauka,
nao upepo wa kisulisuli
huwapeperusha kama makapi.
25“Utanilinganisha mimi na nani?
Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.
26Inueni macho yenu mtazame mbinguni:
Ni nani aliyeumba hivi vyote?
Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine
na kuziita kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,
hakuna hata mojawapo inayokosekana.
27Kwa nini unasema, ee Yakobo,
nanyi ee Israeli, kulalamika,
“Njia yangu imefichwa Mwenyezi Mungu asiione,
Mungu wangu hajali shauri langu?”
28Je wewe, hufahamu?
Je wewe, hujasikia?
Mwenyezi Mungu ni Mungu wa milele,
Muumba wa miisho ya dunia.
Hatachoka wala kulegea,
wala hakuna hata mmoja
awezaye kuupima ufahamu wake.
29Huwapa nguvu waliolegea
na huongeza nguvu za wadhaifu.
30Hata vijana huchoka na kulegea,
nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,
31bali wale wamtumainio Mwenyezi Mungu
atafanya upya nguvu zao.
Watapaa juu kwa mabawa kama tai;
watapiga mbio wala hawatachoka,
watatembea kwa miguu wala hawatazimia.
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 40: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.