Yakobo 2
2
Onyo kuhusu upendeleo
1Ndugu zangu, waumini katika imani ya Bwana wetu wa utukufu, Isa Al-Masihi, hawapaswi kuwa na upendeleo. 2Je, ikiwa mtu anakuja katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, na kisha akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi yaliyochakaa. 3Mkimpa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,” 4je, hamjabagua kati yenu wenyewe na kuwa mahakimu wenye mawazo maovu?
5Ndugu zangu, sikilizeni: Je, si Mungu huwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi ufalme aliowaahidi wale wanaompenda? 6Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani? 7Je, si wao wanalikufuru jina lile bora sana mliloitiwa?
8Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko, isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,”#2:8 Walawi 19:18 mnafanya vyema. 9Lakini mkiwapendelea watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa wakosaji. 10Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote. 11Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,”#2:11 Kutoka 20:14; Kumbukumbu 5:18 alisema pia, “Usiue.”#2:11 Kutoka 20:13; Kumbukumbu 5:17 Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.
12Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru. 13Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.
Imani na matendo
14Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa? 15Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula, 16naye mmoja wenu akamwambia, “Nenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini? 17Vivyo hivyo, imani peke yake, kama haikuambatana na matendo, imekufa.
18Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”
Nioneshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonesha imani yangu kwa matendo. 19Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani wanaamini hivyo na kutetemeka.
20Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu? 21Je, Ibrahimu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaka madhabahuni? 22Unaona jinsi imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda. 23Kwa njia hiyo likatimizwa andiko lisemalo, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki,”#2:23 Mwanzo 15:6 naye akaitwa rafiki wa Mungu. 24Mnaona kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.
25Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba: je, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine? 26Kama vile mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.
Iliyochaguliwa sasa
Yakobo 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.