Waamuzi 19
19
Mlawi na suria wake
1Katika siku hizo, Waisraeli hawakuwa na mfalme.
Basi Mlawi mmoja aliyeishi sehemu za mbali katika nchi ya vilima ya Efraimu, akamchukua suria mmoja kutoka Bethlehemu ya Yuda. 2Lakini suria wake akafanya ukahaba, akamwacha na kurudi nyumbani mwa baba yake huko Bethlehemu ya Yuda. Baada ya kukaa huko kwa muda wa miezi minne, 3mume wake akaenda kumsihi arudi. Alienda na mtumishi wake na punda wawili. Yule mwanamke akamkaribisha nyumbani mwa baba yake, naye baba yake alipomwona akamkaribisha kwa furaha. 4Baba mkwe wake, yaani baba yake yule msichana, akamsihi akae. Hivyo akakaa na huyo baba mkwe wake kwa siku tatu, wakila na kunywa, na kulala huko.
5Siku ya nne wakaamka mapema naye akajiandaa kuondoka, lakini baba wa yule msichana akamwambia mkwewe, “Ujiburudishe kwa kitu cha kula, ndipo uweze kwenda.” 6Basi wakaketi wote wawili ili kula na kunywa pamoja. Baadaye baba wa msichana akamwambia, “Tafadhali ubakie usiku huu upate kujifurahisha.” 7Basi yule mtu alipotaka kuondoka, baba mkwe wake akamsihi, hivyo akabaki usiku ule. 8Asubuhi ya siku ya tano, alipoamka ili aondoke, baba wa yule msichana akamwambia, “Jiburudishe nafsi yako. Ngoja hadi alasiri!” Kwa hiyo wote wawili wakala chakula pamoja.
9Kisha yule mtu alipoinuka aende zake pamoja na suria wake na mtumishi wake, baba mkwe wake, yaani baba wa yule msichana, akamwambia, “Tazama sasa jioni inakaribia. Ulale hapa, usiku unakaribia. Ukae, ukajifurahishe nafsi yako. Kesho unaweza kuamka asubuhi na mapema uende nyumbani kwako.” 10Lakini akakataa kulala tena, akaondoka na kuelekea Yebusi (ndio Yerusalemu), akiwa na punda wake wawili waliotandikwa, pamoja na suria wake.
11Alipokaribia Yebusi na usiku ukiwa umekaribia, mtumishi akamwambia bwana wake, “Haya sasa natuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo.”
12Lakini bwana wake akamjibu, “Hapana. Hatutaingia kwenye mji wa kigeni, ambao watu wake si Waisraeli. Tutaendelea hadi Gibea.” 13Tena akasema, “Haya, tujitahidi tufike Gibea au Rama, nasi tutalala katika mji huo.” 14Hivyo wakaendelea na safari, nalo jua likazama walipokaribia Gibea ya Benyamini. 15Wakageuka ili kuingia na kulala Gibea. Wakaingia humo, wakaketi kwenye uwanja wa mji, wala hakuna mtu yeyote aliyewakaribisha kwake ili wapate kulala.
16Jioni ile, mzee mmoja toka nchi ya vilima ya Efraimu, aliyekuwa anaishi huko Gibea (watu wa sehemu ile walikuwa Wabenyamini), akarudi kutoka kwenye kazi zake za shamba. 17Alipotazama na kuwaona hao wasafiri katika uwanja wa mji, yule mzee akawauliza, “Ninyi mnaenda wapi? Nanyi mmetoka wapi?”
18Akamwambia, “Tumepita kutoka Bethlehemu ya Yuda, tunaelekea katika nchi ya vilima ya Efraimu ninakoishi. Nilienda Bethlehemu ya Yuda na sasa ninaenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu yeyote aliyenikaribisha katika nyumba yake. 19Tunazo nyasi na chakula cha punda wetu, pia mkate na divai kwa ajili yetu sisi watumishi wako: mimi, mtumishi wako mwanamke, pamoja na huyu kijana tuliye naye. Hatuhitaji kitu zaidi.”
20Yule mzee akawaambia, “Amani iwe kwenu! Karibuni nyumbani mwangu. Nitawapa mahitaji yenu yote, ila tu msilale katika uwanja huu.” 21Hivyo akamwingiza nyumbani mwake na kuwalisha punda wake. Baada ya kunawa miguu yao, wakala na kunywa.
22Walipokuwa wakijiburudisha, wanaume waovu wa mji huo wakaizingira ile nyumba. Wakagonga mlango na kusema kwa sauti kuu kwa yule mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanaume aliyeingia kwako, tupate kumlawiti.”
23Yule mwenye nyumba akatoka nje na kuwaambia, “Hapana, ndugu zangu, msiwe waovu namna hii, ninawasihi. Kwa kuwa huyu mwanaume ni mgeni wangu, msifanye jambo hili la aibu. 24Tazameni, hapa yupo binti yangu ambaye ni bikira, na suria wa mtu huyu. Nitawatoleeni hawa sasa, mkawatwae kwa nguvu na kuwafanyia lolote mtakalo. Lakini kwa mwanaume huyu msimfanyie jambo ovu hivyo.”
25Lakini wale wanaume hawakumsikiliza. Hivyo yule mwanaume akamtoa yule suria wake nje kwa wale watu, nao wakambaka na kumnajisi usiku kucha hadi asubuhi. Kulipoanza kupambazuka, wakamwachia aende. 26Alfajiri yule mwanamke akarudi kwenye ile nyumba bwana wake alikokuwa, akaanguka chini mlangoni, akalala pale hata kulipopambazuka.
27Bwana wake alipoamka asubuhi na kufungua mlango wa nyumba na kutoka nje ili kuendelea na safari yake, tazama, yule suria wake alikuwa ameangukia penye ingilio la nyumba, mikono yake ikiwa penye kizingiti. 28Akamwambia yule suria, “Inuka, twende.” Lakini hakujibu. Yule bwana akamwinua, akampandisha juu ya punda wake, na wakaondoka kwenda nyumbani.
29Alipofika nyumbani, akachukua kisu na kumkatakata yule suria kiungo kwa kiungo, vipande kumi na mbili, na kuvipeleka katika sehemu zote za Israeli. 30Kila mtu aliyeona akasema, “Jambo la namna hii halijaonekana wala kutendeka, tangu Waisraeli walipopanda kutoka Misri. Fikirini juu ya jambo hili! Tafakarini juu ya jambo hili! Tuambieni tufanye nini!”
Iliyochaguliwa sasa
Waamuzi 19: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.