39
1Katika mwaka wa tisa wa utawala wa Mfalme Sedekia wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu na akauzingira. 2Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne wa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia, ukuta wa mji ulibomolewa. 3Kisha maafisa wote wa mfalme wa Babeli wakaja na kuketi kwenye Lango la Kati: Nergal-Shareza wa Samgari, Nebo-Sarsekimu afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa mwenye cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli. 4Mfalme Sedekia wa Yuda na askari wote walipowaona, wakakimbia na kuondoka mjini usiku kwa njia ya bustani ya mfalme, kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili, wakaelekea Araba#39:4 yaani Bonde la Yordani.
5Lakini jeshi la Wakaldayo wakawafuatia na kumpata Sedekia katika nchi tambarare za Yeriko. Wakamkamata na kumpeleka kwa Nebukadneza mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ambapo alimtangazia hukumu. 6Huko Ribla, mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake, na pia akawaua wakuu wote wa Yuda. 7Kisha akayang’oa macho ya Sedekia na kumfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
8Jeshi la Wakaldayo likachoma moto jumba la kifalme na nyumba za watu, na kuzibomoa kuta za Yerusalemu. 9Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme akawachukua na kuwapeleka uhamishoni Babeli watu waliokuwa wamebaki ndani ya mji, pamoja na wale waliokuwa wamejisalimisha kwake, na watu wengine wote. 10Lakini Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi aliwabakiza baadhi ya watu maskini katika nchi ya Yuda, ambao hawakuwa na kitu. Naye wakati huo akawapa mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
11Basi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa ametoa maagizo kuhusu Yeremia kupitia Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme akisema: 12“Mchukue umtunze. Usimdhuru, lakini umfanyie chochote anachotaka.” 13Basi Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi, Nebushazbani afisa mkuu, Nergal-Shareza afisa wa cheo cha juu, na maafisa wengine wote wa mfalme wa Babeli 14wakatuma watu kumwondoa Yeremia kutoka ua wa walinzi. Wakamkabidhi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ili amrudishe nyumbani mwake. Kwa hiyo akabaki miongoni mwa watu wake mwenyewe.
15Yeremia alipokuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia kusema: 16“Nenda ukamwambie Ebed-Meleki Mkushi, ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Ninakaribia kutimiza maneno yangu dhidi ya mji huu kwa maafa, wala si kwa mema. Wakati huo, hayo yatatimizwa mbele ya macho yako. 17Lakini siku hiyo nitakuokoa, asema Mwenyezi Mungu; hutatiwa mikononi mwa wale unaowaogopa. 18Nitakuokoa; hutaanguka kwa upanga, maisha yako yatakuwa salama, kwa sababu unanitumaini, asema Mwenyezi Mungu.’ ”