40
Yeremia aachiwa huru
1Neno likamjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli. 2Mkuu wa askari walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aliamuru maafa haya kutokea mahali hapa. 3Sasa Mwenyezi Mungu ameyaleta haya, amefanya sawasawa na alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu na hamkumtii. 4Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Ukiona ni vema, twende pamoja hadi Babeli; nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.” 5Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.”
Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake. 6Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.
Gedalia auawa
(2 Wafalme 25:22-26)
7Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli, 8wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 9Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akaapa ili kuwatia moyo, wao na watu wao. Akasema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu. 10Mimi mwenyewe nitakaa Mispa ili kuwawakilisha mbele ya Wakaldayo wanaotujia, lakini ninyi mtavuna divai, matunda ya kiangazi na mafuta, nanyi mtaweka katika vyombo vyenu vya kuhifadhia, na kuishi katika miji mliyojitwalia.”
11Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, Edomu na nchi nyingine zote waliposikia kwamba mfalme wa Babeli ameacha mabaki ya watu katika Yuda na amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kuwa mtawala wao, 12wakarudi wote katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mispa, kutoka nchi zote ambazo walikuwa wametawanywa. Nao wakavuna divai na matunda tele wakati wa kiangazi.
13Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi wakamjia Gedalia huko Mispa 14na kumwambia, “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini.
15Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia Gedalia kwa siri huko Mispa, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, wala hakuna atakayejua. Kwa nini akuue na kusababisha Wayahudi wote waliokuzunguka watawanyike, na mabaki wa Yuda waangamie?”
16Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo hilo! Unalosema kuhusu Ishmaeli si kweli.”