Yohana 1:1-18
Yohana 1:1-18 NENO
Hapo mwanzo alikuwako Neno, naye huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kupitia kwake, na hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa pasipo yeye. Ndani yake kulikuwa na uzima, nao huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda. Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yahya. Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini. Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni. Huyo Neno alikuwako ulimwenguni, na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. Bali wote waliompokea, yaani wale walioliamini jina lake, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Hawa hawakuzaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu. Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. Yahya alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ ” Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli zimekuja kupitia Isa Al-Masihi. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba, ndiye ambaye amemdhihirisha.