Yohane 1:1-18
Yohane 1:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
Yohane 1:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe. Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
Yohane 1:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
Yohane 1:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda. Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni. Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu. Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli. Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ ” Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo. Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.