Yohana 12:27-36
Yohana 12:27-36 NENO
“Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii’? Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu. Baba, litukuze jina lako.” Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.” Umati ule wa watu waliokuwa mahali pale waliisikia ile sauti, nao wakasema hiyo ilikuwa sauti ya radi; wengine wakasema malaika ameongea naye. Isa akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu. Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.” Isa aliyasema haya akionesha ni kifo gani atakachokufa. Umati ule wa watu wakapaza sauti, wakasema, “Tumesikia kutoka Torati kwamba Al-Masihi adumu milele; hivyo wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?” Ndipo Isa akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingali pamoja nanyi. Nendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakoenda. Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Isa aliondoka, akajificha wasimwone.