Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 14:15-31

Yohana 14:15-31 NEN

“Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima, naja kwenu. Bado kitambo kidogo ulimwengu hautaniona tena, ila ninyi mtaniona, kwa kuwa mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Wakati huo mtajua ya kuwa mimi niko ndani ya Baba na ninyi mko ndani yangu na mimi niko ndani yenu. Yeyote mwenye amri zangu na kuzishika ndiye anipendaye, naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma. “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope. “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru. “Haya inukeni; twendeni zetu.