Yohana 2:1-12
Yohana 2:1-12 NEN
Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Yesu alikuwepo pale. Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia. Divai ilipokwisha, mama yake Yesu akamwambia, “Wameishiwa na divai.” Yesu akamwambia, “Mwanamke, nina nini nawe? Saa yangu haijawadia.” Mama yake akawaambia wale watumishi, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.” Basi ilikuwepo mitungi sita ya kuhifadhia maji iliyotengenezwa kwa mawe kwa ajili ya kujitakasa kwa desturi ya Kiyahudi; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu. Yesu akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi mpaka juu. Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo, mpelekeeni mkuu wa meza.” Hivyo wakachota, wakampelekea. Yule mkuu wa meza akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilika kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji wao walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando akamwambia, “Watu wote hutoa kwanza divai nzuri, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa vya kutosha, lakini wewe umeiweka ile nzuri kupita zote mpaka sasa.” Huu, ndio uliokuwa muujiza wa kwanza Yesu aliofanya Kana ya Galilaya. Hivyo Yesu alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini. Baada ya hayo, Yesu pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka mpaka Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.