Yohana 8:12-30
Yohana 8:12-30 NEN
Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.” Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu yeyote. Lakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma. Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti. Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.” Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.” Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia. Yesu akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi ninyi hamwezi kuja.” Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?” Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini, mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu, kwa maana msipoamini ya kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.” Wakamuuliza, “Wewe ni nani?” Naye Yesu akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo. Nina mambo mengi ya kusema juu yenu na mengi ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kweli, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.” Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia juu ya Baba yake wa Mbinguni. Kisha Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua juu Mwana wa Adamu, ndipo mtakapojua kuwa, ‘Mimi ndiye yule niliyesema na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu bali ninasema yale tu ambayo Baba yangu amenifundisha. Yeye aliyenituma yu pamoja nami, hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.’ ” Wengi waliomsikia Yesu akisema maneno haya wakamwamini.