Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 8:12-30

Yohana 8:12-30 NENO

Kisha Isa akasema nao tena, akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata, hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.” Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki, kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.” Isa akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli, kwa sababu najua nilikotoka na ninakoenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakoenda. Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu; mimi simhukumu mtu yeyote. Lakini hata nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma. Imeandikwa katika Torati yenu kwamba ushahidi wa watu wawili ni thabiti. Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.” Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?” Isa akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.” Isa alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia. Isa akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kuja.” Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?” Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini; mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu; mimi si wa ulimwengu huu. Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu; kwa maana msipoamini kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.” Wakamuuliza, “Wewe ni nani?” Naye Isa akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo. Nina mambo mengi ya kusema kuwahusu ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kuaminika, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.” Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia kuhusu Baba yake wa Mbinguni. Kisha Isa akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua Mwana wa Adamu juu, ndipo mtajua kuwa mimi ndiye yule niliyesema, na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu, bali ninasema yale tu Baba yangu amenifundisha. Yeye aliyenituma yu pamoja nami; hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.” Wengi waliomsikia Isa akisema maneno haya wakamwamini.