Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 8:31-47

Yohana 8:31-47 NENO

Kisha Isa akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Ndipo mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru.” Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Ibrahimu, nasi hatujakuwa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?” Isa akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli. Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Ibrahimu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu. Ninasema yale niliyoyaona nikiwa mbele za Baba yangu, nanyi mnafanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.” Wakajibu, “Baba yetu ni Ibrahimu.” Isa akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Ibrahimu, mngefanya mambo yale aliyofanya Ibrahimu. Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya jambo la namna hii. Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.” Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.” Isa akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. Ninyi ni watoto wa baba yenu, ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli, maana hamna kweli ndani yake. Anaposema uongo, yeye husema lugha yake ya asili kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. Lakini kwa sababu nimewaambia kweli, hamkuniamini! Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”