Yohana 9:18-41
Yohana 9:18-41 NENO
Wale Wayahudi hawakuamini ya kuwa mtu huyo alikuwa kipofu akapata kuona, hadi walipowaita wazazi wake. Wakawauliza, “Je, huyu ni mtoto wenu, ambaye mnasema alizaliwa kipofu? Imekuwaje basi sasa anaona?” Wazazi wake wakajibu, “Tunajua ya kuwa huyu ni mtoto wetu na ya kuwa alizaliwa kipofu. Lakini hatujui jinsi anavyoweza kuona sasa, wala hatujui ni nani aliyemfungua macho yake. Muulizeni; yeye ni mtu mzima na anaweza kujieleza mwenyewe.” Wazazi wake walisema hivi kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi, kwani walikuwa wamekubaliana kuwa mtu yeyote atakayemkiri Isa kuwa ndiye Al-Masihi atafukuzwa kutoka sinagogi. Kwa hiyo wazazi wake wakasema, “Yeye ni mtu mzima. Muulizeni.” Hivyo kwa mara ya pili wakamwita yule aliyekuwa kipofu, nao wakamwambia, “Mpe Mungu utukufu! Sisi tunafahamu kuwa mtu huyu aliyekuponya ni mwenye dhambi.” Akawajibu, “Mimi sijui kama yeye ni mwenye dhambi. Lakini jambo moja ninalojua, nilikuwa kipofu na sasa ninaona.” Wakamuuliza, “Alikufanyia nini? Aliyafumbuaje macho yako?” Akawajibu, “Tayari nimekwisha kuwaambia, nanyi hamtaki kunisikiliza. Mbona mnataka kusikia tena? Je, ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake?” Ndipo wakamtukana na kusema, “Wewe ndiwe mwanafunzi wake! Sisi ni wanafunzi wa Musa. Tunajua kwamba Mungu alisema na Musa, lakini mtu huyu hatujui anakotoka.” Yule mtu akawajibu, “Hili ni jambo la ajabu! Hamjui anakotoka, naye amenifungua macho yangu! Tunajua ya kuwa Mungu hawasikilizi wenye dhambi, lakini huwasikiliza wote wanaomcha na kumtii. Tangu zamani hatujasikia kwamba mtu amemponya yeyote aliyezaliwa kipofu. Kama huyu mtu hakutoka kwa Mungu, asingeweza kufanya lolote.” Wakamjibu, “Wewe ulizaliwa katika dhambi kabisa, nawe unajaribu kutufundisha?” Wakamfukuza atoke nje. Isa aliposikia kuwa wamemfukuza atoke nje yule mtu aliyemfumbua macho, alimkuta, akamuuliza, “Je, unamwamini Mwana wa Adamu?” Yule mtu akamjibu, “Yeye ni nani, Bwana? Niambie ili nipate kumwamini.” Isa akamjibu, “Umekwisha kumwona; naye anayezungumza nawe, ndiye.” Yule mtu akasema, “Bwana, naamini.” Naye akamwabudu. Isa akasema, “Nimekuja ulimwenguni humu kwa ajili ya kuhukumu, ili wale walio vipofu wapate kuona, nao wale wanaoona wawe vipofu.” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa karibu naye wakamsikia na kumwambia, “Je, kweli sisi ni vipofu?” Isa akawajibu, “Kama mngekuwa vipofu kweli, msingekuwa na hatia ya dhambi, lakini kwa kuwa mnasema, ‘Tunaona,’ basi mna hatia.