1
Sehemu ya kwanza: Habari za awali
(Ayubu 1–2)
Ayubu na jamaa yake
1Katika nchi ya Usi paliishi mtu ambaye aliitwa Ayubu. Mtu huyu alikuwa hana hatia, naye alikuwa mkamilifu; alimcha Mungu na kuepukana na uovu. 2Alikuwa na wana saba na binti watatu, 3naye alikuwa na kondoo elfu saba, ngamia elfu tatu, jozi mia tano za maksai, na punda mia tano, tena alikuwa na idadi kubwa ya watumishi. Alikuwa mtu maarufu sana miongoni mwa watu wa Mashariki.
4Wanawe walikuwa na desturi ya kufanya karamu katika nyumba zao kwa zamu, nao wangewaalika dada zao watatu ili kula na kunywa pamoja nao. 5Kipindi cha karamu kilipomalizika, Ayubu angetuma waitwe na kuwafanyia utakaso. Angetoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya kila mmoja wao asubuhi na mapema, akifikiri, “Pengine wanangu wametenda dhambi na kumlaani Mungu mioyoni mwao.” Hii ilikuwa ndiyo desturi ya kawaida ya Ayubu.
Jaribu la kwanza la Ayubu
6Siku moja wana wa Mungu#1:6 wana wa Mungu hapa ina maana malaika au viumbe vya mbinguni walienda kujionesha mbele za Mwenyezi Mungu. Shetani#1:6 yaani mshtaki wa watakatifu naye akaja pamoja nao. 7Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”
Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.”
8Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu, na kuepukana na uovu.”
9Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Je, Ayubu anamcha Mungu bure? 10Je, wewe hukumzingira pande zote, yeye na watu wa nyumbani mwake, pamoja na kila kitu alicho nacho? Kazi za mikono yake umezibariki, na hivyo makundi yake ya kondoo na mbuzi pamoja na ya wanyama yameenea katika nchi nzima. 11Lakini nyoosha mkono wako na kupiga kila kitu alicho nacho, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
12Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Vema sana, kwa hiyo, kila kitu alicho nacho kiko mikononi mwako, lakini huyo mtu mwenyewe usimguse hata kwa kidole.”
Ndipo Shetani akatoka mbele za Mwenyezi Mungu.
13Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 14akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, 15Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!”
16Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!”
17Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari.”
18Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako wa kiume na wa kike walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, 19ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!”
20Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akasujudu na kuabudu, 21akasema:
“Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi,
nami nitaondoka uchi#1:21 au nitarudi huko uchi,
Mwenyezi Mungu alinipa,
naye Mwenyezi Mungu ameviondoa;
jina la Mwenyezi Mungu litukuzwe.”
22Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa kumlaumu Mungu kwa kufanya ubaya.