Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 2

2
Jaribu la pili la Ayubu
1Siku nyingine wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za Mwenyezi Mungu. Shetani naye akaja pamoja nao kujionesha mbele zake. 2Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”
Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.”
3Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”
4Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake. 5Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
6Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Vema sana; kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”
7Basi Shetani akatoka mbele za Mwenyezi Mungu, naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa. 8Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho, huku akiketi kwenye majivu.
9Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”
10Akamjibu, “Unazungumza kama mwanamke mpumbavu#2:10 maana yake kupungukiwa maadili. Je, tupokee mema kutoka kwa Mungu, bali tusipokee mabaya?”
Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.
Rafiki watatu wa Ayubu
11Basi rafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia kuhusu taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga kutoka nyumbani mwao, wakakutana ili kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. 12Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. 13Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia