Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 12

12
Hotuba ya nne ya Ayubu
Ayubu anajibu: Mimi ni mtu wa kuchekwa
1Ndipo Ayubu akajibu:
2“Bila shaka ninyi ndio watu,
nayo hekima itakoma mtakapokufa!
3Lakini mimi ninao ufahamu kama ninyi;
mimi si duni kwenu.
Ni nani asiyejua mambo haya yote?
4“Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu,
ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu:
mimi ni mtu wa kuchekwa tu,
ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!
5Wanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba
kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.
6Mahema ya wanyang’anyi hayasumbuliwi,
wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama:
wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.
7“Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,
au ndege wa angani, nao watawaambia;
8au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,
au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.
9Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua
kwamba mkono wa Mwenyezi Mungu ndio uliofanya hili?
10Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,
na pumzi ya wanadamu wote.
11Je, sikio haliyajaribu maneno
kama vile ulimi uonjavyo chakula?
12Je, hekima haipatikani kwa wazee?
Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?
13“Hekima na nguvu ni vya Mungu;
shauri na ufahamu ni vyake yeye.
14Kile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena;
mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.
15Akizuia maji, huwa pana ukame;
akiyaachia maji, huharibu nchi.
16Kwake kuna nguvu na ushindi;
anayedanganywa na anayedanganya, wote wawili ni wake.
17Yeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara,
naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.
18Huondoa pingu zilizofungwa na wafalme,
na kuwafunga mishipi ya kiunoni.
19Huwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara,
na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.
20Hunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika,
na kuondoa busara ya wazee.
21Huwadharau wanaoheshimika,
na kuwavua silaha wenye nguvu.
22Hufunua mambo ya ndani ya gizani,
na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.
23Huyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza;
hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.
24Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao;
huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.
25Hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga;
huwafanya wapepesuke kama walevi.

Iliyochaguliwa sasa

Ayubu 12: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia