Ayubu 28:12-28
Ayubu 28:12-28 NEN
“Lakini hekima inaweza kupatikana wapi? Ufahamu unakaa wapi? Mwanadamu hatambui thamani yake; haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai. Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’; bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’ Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote, wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha. Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri, kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa. Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu. Marijani na yaspi hazistahili kutajwa; thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu. Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi. “Ni wapi basi hekima itokako? Ufahamu hukaa wapi? Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai, imesitiriwa hata kwa ndege wa angani. Uharibifu na Mauti husema, ‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’ Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa, kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia na huona kila kitu chini ya mbingu. Alipofanyiza nguvu za upepo na kuyapima maji, alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua na njia kwa ajili ya umeme wa radi, ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake, akaithibitisha na kuihakikisha. Naye Mungu akamwambia mwanadamu, ‘Kumcha BWANA: hiyo ndiyo hekima, nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”