Yobu 28:12-28
Yobu 28:12-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bali hekima itapatikana wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? Mwanadamu hajui thamani yake, Wala haionekani katika nchi ya walio hai. Vilindi vyasema, Haimo ndani yangu; Na bahari yasema, Haiko kwangu. Haipatikani kwa dhahabu, Wala fedha haitapimwa iwe thamani yake. Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri, Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti ya samawi. Dhahabu na vioo haviwezi kulinganishwa nayo; Wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi. Havitatajwa fedhaluka wala bilauri; Naam, kima cha hekima chapita marijani. Yakuti ya rangi ya manjano ya Kushi haitasawazishwa nayo, Wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi. Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani. Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu. Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake. Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza. Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu.
Yobu 28:12-28 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini hekima itapatikana wapi? Ni mahali gani panapopatikana maarifa? Hakuna mtu ajuaye thamani ya hekima, wala hekima haipatikani nchini mwa walio hai. Vilindi vyasema, ‘Hekima haimo kwetu,’ na bahari yasema, ‘Haiko kwangu.’ Hekima haiwezi kupatikana kwa dhahabu, wala kwa kupima kiasi kingi cha fedha. Haiwezi kupimwa kwa dhahabu ya Ofiri, wala kwa vito vya Sardoniki au vya rangi ya samawati, dhahabu au kioo havilingani nayo, wala haiwezi kubadilishwa na vito vya dhahabu safi. Hekima ina thamani kuliko matumbawe na marijani, thamani yake yashinda thamani ya lulu. Topazi ya Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kupewa bei ya dhahabu safi. “Basi, hekima yatoka wapi? Ni wapi panapopatikana maarifa? Imefichika machoni pa viumbe vyote hai, na ndege wa angani hawawezi kuiona. Abadoni na Kifo wasema, ‘Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.’ “Mungu aijua njia ya hekima, anajua mahali inapopatikana. Maana yeye huona mpaka upeo wa dunia, huona kila kitu chini ya mbingu. Alipoupa upepo uzito wake, na kuyapimia maji mipaka yake; alipoamua mvua inyeshe wapi, umeme na radi vipite wapi; hapo ndipo alipoiona hekima na kuitangaza, aliisimika na kuichunguza.” Kisha Mungu akamwambia mwanadamu: “Tazama! Kumcha Bwana ndio hekima; na kujitenga na uovu ndio maarifa.”
Yobu 28:12-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bali hekima itapatikana wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? Mwanadamu hajui thamani yake, Wala haionekani katika nchi ya walio hai. Vilindi vyasema, Haimo ndani yangu; Na bahari yasema, Haiko kwangu. Haipatikani kwa dhahabu, Wala fedha haitapimwa iwe thamani yake. Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri, Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti samawi. Dhahabu na vioo haviwezi kulinganishwa nayo; Wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi. Havitatajwa fedhaluka wala bilauri; Naam, kima cha hekima chapita marijani. Yakuti ya rangi ya manjano ya Kushi haitasawazishwa nayo, Wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi. Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani. Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu. Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake. Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza. Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu.
Yobu 28:12-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Lakini hekima inaweza kupatikana wapi? Ufahamu unakaa wapi? Mwanadamu hatambui thamani yake; haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai. Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’; bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’ Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote, wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha. Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri, kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa. Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu. Marijani na yaspi hazistahili kutajwa; thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu. Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi. “Ni wapi basi hekima itokako? Ufahamu hukaa wapi? Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai, imesitiriwa hata kwa ndege wa angani. Uharibifu na Mauti husema, ‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’ Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa, kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia na huona kila kitu chini ya mbingu. Alipofanyiza nguvu za upepo na kuyapima maji, alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua na njia kwa ajili ya umeme wa radi, ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake, akaithibitisha na kuihakikisha. Naye Mungu akamwambia mwanadamu, ‘Kumcha BWANA: hiyo ndiyo hekima, nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”