Yobu 28:12-28
Yobu 28:12-28 BHN
“Lakini hekima itapatikana wapi? Ni mahali gani panapopatikana maarifa? Hakuna mtu ajuaye thamani ya hekima, wala hekima haipatikani nchini mwa walio hai. Vilindi vyasema, ‘Hekima haimo kwetu,’ na bahari yasema, ‘Haiko kwangu.’ Hekima haiwezi kupatikana kwa dhahabu, wala kwa kupima kiasi kingi cha fedha. Haiwezi kupimwa kwa dhahabu ya Ofiri, wala kwa vito vya Sardoniki au vya rangi ya samawati, dhahabu au kioo havilingani nayo, wala haiwezi kubadilishwa na vito vya dhahabu safi. Hekima ina thamani kuliko matumbawe na marijani, thamani yake yashinda thamani ya lulu. Topazi ya Kushi haiwezi kulinganishwa nayo, wala haiwezi kupewa bei ya dhahabu safi. “Basi, hekima yatoka wapi? Ni wapi panapopatikana maarifa? Imefichika machoni pa viumbe vyote hai, na ndege wa angani hawawezi kuiona. Abadoni na Kifo wasema, ‘Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.’ “Mungu aijua njia ya hekima, anajua mahali inapopatikana. Maana yeye huona mpaka upeo wa dunia, huona kila kitu chini ya mbingu. Alipoupa upepo uzito wake, na kuyapimia maji mipaka yake; alipoamua mvua inyeshe wapi, umeme na radi vipite wapi; hapo ndipo alipoiona hekima na kuitangaza, aliisimika na kuichunguza.” Kisha Mungu akamwambia mwanadamu: “Tazama! Kumcha Bwana ndio hekima; na kujitenga na uovu ndio maarifa.”