Yobu 28
28
Sifa za hekima
1“Hakika kuna machimbo ya fedha,
na mahali ambako dhahabu husafishwa.
2Watu huchimba chuma ardhini,
huyeyusha shaba kutoka mawe ya madini.
3Wachimba migodi huleta taa gizani,
huchunguza vina vya ardhi
na kuchimbua mawe yenye madini gizani.
4Binadamu huchimba mashimo mbali na makazi ya watu,
mbali na watu mahali kusipofikika,
wachimba madini huninginia wamefungwa kamba.
5Kutoka udongoni chakula hupatikana,
lakini chini yake kila kitu huvurugwa kwa moto.
6Katika mawe yake ndimo vilimo vito vya rangi ya samawati
na udongo wake una vumbi la dhahabu.
7“Njia za kwenda kwenye migodi hiyo
hakuna ndege mla nyama azijuaye;
na wala jicho la tai halijaiona.
8Wanyama waendao kwa madaha hawajazikanyaga
wala simba hawajawahi kuzipitia.
9Binadamu huchimbua miamba migumu kabisa,
huichimbua milima na kuiondolea mbali.
10Hupasua mifereji kati ya majabali,
na jicho lake huona vito vya thamani.
11Huziba chemchemi zisitiririke,
na kufichua vitu vilivyofichika.
12 # Taz Sir 1:6; Bar 3:15 “Lakini hekima itapatikana wapi?
Ni mahali gani panapopatikana maarifa?
13 # Taz Bar 3:29-31 Hakuna mtu ajuaye thamani ya hekima,
wala hekima haipatikani nchini mwa walio hai.
14Vilindi vyasema, ‘Hekima haimo kwetu,’
na bahari yasema, ‘Haiko kwangu.’
15Hekima haiwezi kupatikana kwa dhahabu,
wala kwa kupima kiasi kingi cha fedha.
16Haiwezi kupimwa kwa dhahabu ya Ofiri,
wala kwa vito vya Sardoniki au vya rangi ya samawati,
17dhahabu au kioo havilingani nayo,
wala haiwezi kubadilishwa na vito vya dhahabu safi.
18Hekima ina thamani kuliko matumbawe na marijani,
thamani yake yashinda thamani ya lulu.
19Topazi ya Kushi haiwezi kulinganishwa nayo,
wala haiwezi kupewa bei ya dhahabu safi.
20“Basi, hekima yatoka wapi?
Ni wapi panapopatikana maarifa?
21Imefichika machoni pa viumbe vyote hai,
na ndege wa angani hawawezi kuiona.
22Abadoni na Kifo wasema,
‘Tumesikia uvumi wake kwa masikio yetu.’
23 # Taz Bar 3:35-37 “Mungu aijua njia ya hekima,
anajua mahali inapopatikana.
24Maana yeye huona mpaka upeo wa dunia,
huona kila kitu chini ya mbingu.
25Alipoupa upepo uzito wake,
na kuyapimia maji mipaka yake;
26alipoamua mvua inyeshe wapi,
umeme na radi vipite wapi;
27 # Taz Sira 1:9,19 hapo ndipo alipoiona hekima na kuitangaza,
aliisimika na kuichunguza.”
28 # Taz Zab 111:10; Meth 1:7; 9:10 Kisha Mungu akamwambia mwanadamu:
“Tazama! Kumcha Bwana ndio hekima;
na kujitenga na uovu ndio maarifa.”
Iliyochaguliwa sasa
Yobu 28: BHN
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.