Ayubu 29:1-10
Ayubu 29:1-10 NENO
Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema: “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita, zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda, wakati taa yake ilinimulika kichwani, na kwa mwanga wa Mungu nikapita katikati ya giza! Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu, urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu, wakati Mwenyezi bado alikuwa pamoja nami, nao watoto wangu wakawa wamenizunguka, wakati njia yangu ilikuwa imenyeshewa siagi, nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni. “Wakati nilienda kwenye lango la mji na kuketi katika kiwanja, vijana waliniona, wakakaa kando, nao wazee walioketi, wakasimama; wakuu wakaacha kuzungumza, na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao; wenye vyeo wakanyamazishwa, nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.