Ayubu 33:8-22
Ayubu 33:8-22 NEN
“Lakini umesema nikiwa ninakusikia, nami nilisikia maneno yenyewe: ‘Mimi ni safi na sina dhambi; mimi ni safi na sina hatia. Lakini bado Mungu amepata dosari kwangu, naye ananiona kama adui yake. Ananifunga miguu kwa pingu, tena anaziangalia njia zangu zote kwa karibu.’ “Lakini mimi ninakuambia, katika jambo hili wewe una makosa, kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu. Kwa nini unamlalamikia kwamba yeye hamjibu mwanadamu? Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja, au wakati mwingine kwa njia nyingine, ingawa mwanadamu anaweza asielewe. Mungu husema na mwanadamu katika ndoto, katika maono ya usiku, wakati usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu wasinziapo vitandani mwao, anaweza akasemea masikioni mwao, na kuwatia hofu kwa maonyo, ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya na kumwepusha na kiburi, kuiokoa nafsi yake na shimo, uhai wake usiangamizwe kwa upanga. Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake, kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri. Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda, nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika, sasa inatokeza nje. Nafsi yake inakaribia kaburi, nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.