Ayubu 33
33
Elihu amkemea Ayubu
1“Lakini Ayubu, sasa sikiliza maneno yangu;
zingatia kila kitu nitakachosema.
2Karibu nitafungua kinywa changu;
maneno yangu yapo katika ncha ya ulimi wangu.
3Maneno yangu yanatoka katika moyo mnyofu;
midomo yangu hunena kwa uaminifu yale niyajuayo.
4Roho wa Mungu ameniumba;
pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.
5Unijibu basi, kama unaweza;
jiandae kunikabili mimi.
6Mimi ni kama wewe mbele za Mungu;
mimi pia nimetolewa kwenye udongo.
7Huna sababu ya kuniogopa,
wala mkono wangu haupaswi kukulemea.
8“Lakini umesema nikiwa ninakusikia,
nami nilisikia maneno yenyewe:
9‘Mimi ni safi na sina dhambi;
mimi ni safi na sina hatia.
10Lakini bado Mungu amepata dosari kwangu,
naye ananiona kama adui yake.
11Ananifunga miguu kwa pingu,
tena anaziangalia njia zangu zote kwa karibu.’
12“Lakini mimi ninakuambia,
katika jambo hili wewe una makosa,
kwa maana Mungu ni mkuu
kuliko mwanadamu.
13Kwa nini unamlalamikia
kwamba yeye hamjibu mwanadamu?
14Kwa kuwa Mungu husema,
wakati huu kwa njia moja,
au wakati mwingine kwa njia nyingine,
ingawa mwanadamu anaweza asielewe.
15Mungu husema na mwanadamu katika ndoto,
katika maono ya usiku,
wakati usingizi mzito uwaangukiapo
wanadamu wasinziapo vitandani mwao,
16anaweza akasemea masikioni mwao,
na kuwatia hofu kwa maonyo,
17ili kumgeuza mtu kutoka kutenda mabaya
na kumwepusha na kiburi,
18kuiokoa nafsi yake na shimo,
uhai wake usiangamizwe kwa upanga.
19Mtu anaweza kutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake,
kwa dhiki za mfululizo katika mifupa yake,
20kiasi kwamba maisha yake yenyewe yanakataa chakula
nayo nafsi yake ikakichukia kabisa hata chakula kizuri.
21Nyama ya mwili wake huisha kwa kukonda,
nayo mifupa yake ambayo mwanzoni ilikuwa imefichika,
sasa inatokeza nje.
22Nafsi yake inakaribia kaburi,
nao uhai wake karibu na wajumbe wa kifo.
23“Kama bado kuna malaika upande wake
kama mtetezi, mmoja miongoni mwa elfu,
wa kumwambia mwanadamu lililo jema kwake,
24kumwonea huruma na kusema,
‘Mwokoe asije akatumbukia shimoni;
nimepata ukombozi kwa ajili yake’:
25ndipo nyama ya mwili wake hufanywa mpya kama ya mtoto;
hurudishwa upya kama siku za ujana wake.
26Humwomba Mungu, akapata kibali kwake,
huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha;
Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.
27Ndipo huja mbele za watu na kusema,
‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki,
lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.
28Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni,
nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’
29“Mungu hufanya haya yote kwa mwanadamu;
mara mbili hata mara tatu,
30ili aigeuze nafsi yake toka shimoni,
ili nuru ya uzima imwangazie.
31“Ayubu, zingatia, nisikilize mimi;
nyamaza, nami nitanena.
32Kama unalo lolote la kusema, unijibu;
sema, kwa maana ninataka uonekane huna hatia.
33Lakini kama huna la kusema, basi nisikilize mimi;
nyamaza, nami nitakufundisha hekima.”
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 33: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapistaging.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.