34
Elihu atangaza haki ya Mwenyezi Mungu
1Kisha Elihu akasema:
2“Sikieni maneno yangu, enyi watu wenye hekima;
nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye maarifa.
3Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno
kama vile ulimi uonjavyo chakula.
4Tujichagulie wenyewe yaliyo sawa,
nasi tujifunze pamoja yaliyo mema.
5“Ayubu anasema, ‘Mimi sina hatia,
lakini Mungu ameninyima haki yangu.
6Ingawa niko sawa,
ninaonekana mwongo;
nami ingawa sina kosa,
kidonda changu hakiponi.’
7Ni mtu gani aliye kama Ayubu,
anywaye dharau kama maji?
8Hushirikiana na watenda maovu,
na kuchangamana na watu waovu.
9Kwa kuwa anasema, ‘Haimfaidi mwanadamu kitu chochote
anapojitahidi kumpendeza Mungu.’
10“Hivyo nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye ufahamu.
Kamwe Mungu hatendi uovu,
Mwenyezi hafanyi kosa.
11Humlipa mwanadamu kwa ajili ya lile alilotenda;
huleta juu yake kile ambacho matendo yake yanastahili.
12Ni jambo lisilofikirika kwamba Mungu angefanya makosa,
kwamba Mwenyezi angepotosha hukumu.
13Je, ni nani aliyemtawaza juu ya dunia?
Ni nani aliyemweka kuwa mwangalizi wa ulimwengu wote?
14Kama lilikuwa kusudi la Mungu,
naye akaiondoa Roho yake na pumzi yake,
15wanadamu wote wangeangamia kwa pamoja,
na mtu angerudi mavumbini.
16“Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili;
sikilizeni hili nisemalo.
17Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala?
Je, utamhukumu mwenye haki,
yeye Aliye na Nguvu Zote?
18Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’
nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’
19yeye asiyependelea wakuu,
wala haoneshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini,
kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake?
20Wanakufa ghafula, usiku wa manane;
watu wanatikiswa nao hupita;
wenye nguvu huondolewa
bila mkono wa mwanadamu.
21“Macho yake yanazitazama njia za wanadamu;
anaona kila hatua yao.
22Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa,
ambapo watenda maovu wanaweza kujificha.
23Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana,
ili apate kuja mbele zake kwa hukumu.
24Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi
na kuwaweka wengine mahali pao.
25Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote,
huwaondoa usiku, nao wakaangamia.
26Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao
mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona,
27kwa sababu wameacha kumfuata Mungu,
nao hawakuiheshimu njia yake hata moja.
28Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake,
hivyo akasikia kilio cha wahitaji.
29Lakini akikaa kimya,
ni nani awezaye kumhukumu?
Akiuficha uso wake,
ni nani awezaye kumwona?
Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa,
30ili kumzuia mtu mwovu kutawala,
au wale ambao huwategea watu mitego.
31“Kama mwanadamu akimwambia Mungu,
‘Nimekosa lakini sitatenda dhambi tena.
32Nifundishe nisichoweza kuona;
kama nimekukosea, sitafanya hivyo tena.’
33Je basi, Mungu atakulipa kwa masharti yako,
wakati wewe umekataa kutubu?
Yakupasa wewe uamue, wala si mimi;
sasa niambie lile ulijualo.
34“Watu wenye ufahamu husema,
wenye hekima wanaonisikia huniambia,
35‘Ayubu huongea bila maarifa;
maneno yake hayana busara.’
36Laiti Ayubu angejaribiwa hadi mwisho,
kwa sababu anajibu kama mtu mwovu!
37Kwenye dhambi yake huongeza uasi;
kwa dharau hupiga makofi miongoni mwetu,
na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”