Ayubu 42
42
Sehemu ya tano
(Ayubu 42)
Ayubu anamjibu Mwenyezi Mungu
1Ndipo Ayubu akamjibu Mwenyezi Mungu:
2“Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote,
wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.
3Uliuliza, ‘Ni nani huyu
afichaye mashauri yangu
bila maarifa?’
Hakika nilisema mambo nisiyoyaelewa,
mambo ya ajabu mno
kwangu mimi kuyajua.
4“Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena;
nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’
5Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako,
lakini sasa macho yangu yamekuona.
6Kwa hiyo najidharau mwenyewe,
na kutubu katika mavumbi na majivu.”
Mwisho: Rafiki zake Ayubu wanafedheheshwa
7Baada ya Mwenyezi Mungu kusema mambo haya yote na Ayubu, akamwambia Elifazi Mtemani, “Nina hasira nawe na rafiki zako wawili, kwa sababu hamkusema yaliyo sawa kunihusu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu. 8Basi sasa chukueni mafahali saba na kondoo dume saba mkamwendee mtumishi wangu Ayubu nanyi mkatoe sadaka za kuteketezwa kwa ajili yenu wenyewe. Mtumishi wangu Ayubu atawaombea, nami nitayakubali maombi yake ili nisiwatendee sawasawa na upumbavu wenu. Ninyi hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.” 9Kwa hiyo Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi wakafanya kama Mwenyezi Mungu alivyowaambia; naye Mwenyezi Mungu akayakubali maombi ya Ayubu.
10Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Mwenyezi Mungu akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni. 11Ndipo ndugu zake na dada zake wote, na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni wakaja, wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote Mwenyezi Mungu aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu.
12Mwenyezi Mungu akaibariki sehemu ya mwisho ya maisha ya Ayubu kuliko ile ya kwanza. Alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, ngamia elfu sita, jozi za mafahali elfu moja, na punda jike elfu moja. 13Tena alikuwa na wana saba na binti watatu. 14Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia, na wa tatu Keren-Hapuki. 15Katika nchi ile yote hakukuwa wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao.
16Baada ya hili Ayubu akaishi miaka mia moja na arobaini; akawaona wanawe, na wana wa wanawe hata kizazi cha nne. 17Hivyo Ayubu akafa, akiwa mzee aliyeshiba siku.
Iliyochaguliwa sasa
Ayubu 42: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.