Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoeli 2:1-11

Yoeli 2:1-11 NEN

Pigeni tarumbeta katika Sayuni; pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu. Wote waishio katika nchi na watetemeke, kwa kuwa siku ya BWANA inakuja. Iko karibu, siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na utusitusi. Kama mapambazuko yasambaavyo toka upande huu wa milima hata upande mwingine jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja. Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani wala halitakuwepo tena kamwe kwa vizazi vijavyo. Mbele yao moto unateketeza, nyuma yao miali ya moto inawaka kwa nguvu. Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa lisilofaa: hakuna kitu kinachowaepuka. Wanaonekana kama farasi; wanakwenda mbio kama askari wapanda farasi. Wanatoa sauti kama magari ya vita, wanaporukaruka juu ya vilele vya milima, kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua, kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita. Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu; kila uso unabadilika rangi. Wanashambulia kama wapiganaji wa vita; wanapanda kuta kama askari. Wote wanatembea katika safu, hawapotoshi safu zao. Hakuna anayemsukuma mwenzake; kila mmoja anakwenda mbele moja kwa moja. Wanapita katika vizuizi bila kuharibu safu zao. Wanaenda kasi kuingia mjini; wanakimbia ukutani. Wanaingia ndani ya nyumba; kwa kuingilia madirishani kama wevi. Mbele yao dunia inatikisika, anga linatetemeka, jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota hazitoi mwanga wake tena. BWANA anatoa mshindo wa ngurumo mbele ya jeshi lake; majeshi yake hayana idadi, ni wenye nguvu nyingi wale ambao hutii agizo lake. Siku ya BWANA ni kuu, ni ya kutisha. Ni nani anayeweza kuistahimili?