Yoeli 2:1-11
Yoeli 2:1-11 BHN
Pigeni tarumbeta huko Siyoni; pigeni baragumu juu ya mlima mtakatifu! Tetemekeni enyi wakazi wa Yuda, maana siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja, naam, siku hiyo iko karibu! Hiyo ni siku ya giza na huzuni; siku ya mawingu na giza nene. Jeshi kubwa la nzige linakaribia kama giza linalotanda milimani. Namna hiyo haijapata kuweko kamwe wala haitaonekana tena katika vizazi vyote vijavyo. Kama vile moto uteketezavyo jeshi hilo laharibu kila kitu mbele yake na kuacha nyuma kila kitu kinateketezwa; kabla hawajapita, nchi ni kama bustani ya Edeni, lakini wakisha pita, ni jangwa tupu. Hakuna kiwezacho kuwaepa! Wanaonekana kama farasi, wanashambulia kama farasi wa vita, Wanaporukaruka kwenye vilele vya milima, wanarindima kama magari ya farasi, wanavuma kama mabua makavu motoni. Wamejipanga kama jeshi kubwa tayari kabisa kufanya vita. Wakaribiapo, watu hujaa hofu, nyuso zao zinawaiva. Wanashambulia kama mashujaa wa vita; kuta wanazipanda kama wanajeshi. Wote wanakwenda mbele moja kwa moja, bila hata mmoja wao kubadilisha njia. Hakuna amsukumaye mwenziwe; kila mmoja anafuata mkondo wake. Wanapita kati ya vizuizi vya silaha, wala hakuna kiwezacho kuwazuia. Wanauvamia mji, wanapiga mbio ukutani; wanaziparamia nyumba na kuingia, wanapenya madirishani kama wezi. Nchi inatetemeka mbele yao, mbingu zinatikisika. Jua na mwezi vyatiwa giza, nazo nyota zinaacha kuangaza. Mwenyezi-Mungu anaamuru jeshi lake kwa sauti; askari wake ni wengi mno, wanaomtii hawahesabiki. 2Siku ya Mwenyezi-Mungu kweli ni kuu na ya kutisha sana! Nani atakayeweza kuistahimili?