Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yona 1:7-16

Yona 1:7-16 NENO

Kisha mabaharia wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tupige kura tumtafute anayehusika na maafa haya.” Wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona. Kwa hiyo walimuuliza, “Tuambie, ni nani anayehusika kwa kutuletea tatizo hili lote? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? Nchi yako ni ipi? Wewe ni kutoka taifa lipi?” Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.” Hili liliwaogopesha nao wakamuuliza, “Umefanya nini?” (Walijua alikuwa anamkimbia Mwenyezi Mungu, kwa sababu alishawaambia hivyo.) Bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Kwa hiyo walimuuliza, “Tukutendee nini ili kufanya bahari itulie kwa ajili yetu?” Akawajibu, “Niinueni mnitupe baharini, nayo itakuwa shwari. Ninajua mawimbi haya makubwa yamewatokea kwa ajili ya kosa langu.” Badala yake, wale watu walijitahidi kupiga makasia walivyoweza ili wapate kurudi pwani. Lakini hawakuweza, kwa kuwa bahari ilizidi kuchafuka kuliko mwanzo. Ndipo wakamlilia Mwenyezi Mungu, “Ee Mwenyezi Mungu, tafadhali usituue kwa kumuua mtu huyu. Usituhesabie hatia kwa kumuua mtu asiyekuwa na hatia, kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umefanya kama ilivyokupendeza.” Kisha wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia. Katika jambo hili watu wakamwogopa Mwenyezi Mungu sana, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu na kumwekea nadhiri.