1
Yona amkimbia Mwenyezi Mungu
1Neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Yona mwana wa Amitai: 2“Nenda mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri dhidi yake, kwa sababu uovu wake umefika kwangu.”
3Lakini Yona alimkimbia Mwenyezi Mungu na kuelekea Tarshishi. Alishuka hadi Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda kwenye meli na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia Mwenyezi Mungu.
4Ndipo Mwenyezi Mungu akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini ya kuvunjika. 5Mabaharia wote waliogopa na kila mmoja akamlilia mungu wake mwenyewe. Nao wakatupa mizigo baharini ili meli ipungue uzito.
Lakini Yona alikuwa ameteremkia chumba cha ndani ya meli, ambapo alilala na kupatwa na usingizi mzito. 6Nahodha akamwendea na kusema, “Wewe unawezaje kulala? Amka ukamwite mungu wako! Huenda akatuangalia, tusiangamie.”
7Kisha mabaharia wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tupige kura tumtafute anayehusika na maafa haya.” Wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.
8Kwa hiyo walimuuliza, “Tuambie, ni nani anayehusika kwa kutuletea tatizo hili lote? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? Nchi yako ni ipi? Wewe ni kutoka taifa lipi?”
9Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.”
10Hili liliwaogopesha nao wakamuuliza, “Umefanya nini?” (Walijua alikuwa anamkimbia Mwenyezi Mungu, kwa sababu alishawaambia hivyo.)
11Bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Kwa hiyo walimuuliza, “Tukutendee nini ili kufanya bahari itulie kwa ajili yetu?”
12Akawajibu, “Niinueni mnitupe baharini, nayo itakuwa shwari. Ninajua mawimbi haya makubwa yamewatokea kwa ajili ya kosa langu.”
13Badala yake, wale watu walijitahidi kupiga makasia walivyoweza ili wapate kurudi pwani. Lakini hawakuweza, kwa kuwa bahari ilizidi kuchafuka kuliko mwanzo. 14Ndipo wakamlilia Mwenyezi Mungu, “Ee Mwenyezi Mungu, tafadhali usituue kwa kumuua mtu huyu. Usituhesabie hatia kwa kumuua mtu asiyekuwa na hatia, kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umefanya kama ilivyokupendeza.” 15Kisha wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia. 16Katika jambo hili watu wakamwogopa Mwenyezi Mungu sana, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu na kumwekea nadhiri.
17Lakini Mwenyezi Mungu akamwandaa samaki mkubwa sana kummeza Yona, naye Yona alikuwa ndani ya tumbo la samaki huyo kwa siku tatu, usiku na mchana.