Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 23

23
Yoshua awaaga viongozi
1Baada ya muda mrefu kupita, naye Mwenyezi Mungu akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana, 2akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa. Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana. 3Ninyi wenyewe mmeona kila kitu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewapigania. 4Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi. 5Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaahidi.
6“Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7Msishirikiane na mataifa yaliyobakia kati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8Bali mtashikamana kwa uthabiti na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama vile mmefanya hadi sasa.
9“Mwenyezi Mungu amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, hadi leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu. 10Mtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapigania, kama alivyoahidi. 11Kwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
12“Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia kati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, 13basi mwe na hakika kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa.
14“Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. 15Lakini kama vile kila ahadi njema ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, imekuwa kweli, vivyo hivyo Mwenyezi Mungu ataleta maovu yote kama alivyoonya, hadi awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. 16Mkilivunja agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya Mwenyezi Mungu itawaka dhidi yenu, basi nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”

Iliyochaguliwa sasa

Yoshua 23: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia