Luka 17:11-19
Luka 17:11-19 NEN
Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!” Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika. Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria. Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”