Luka 17:11-19
Luka 17:11-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.
Luka 17:11-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia katika mipaka ya Samaria na Galilaya. Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali. Wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma!” Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika. Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa, alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria. Hapo Yesu akasema, “Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi? Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?” Halafu akamwambia huyo mtu, “Simama, uende zako; imani yako imekuponya.”
Luka 17:11-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Nendeni, mkajioneshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale tisa wako wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, nenda zako, imani yako imekuokoa.
Luka 17:11-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, wakapaza sauti, wakasema, “Yesu, Bwana, tuhurumie!” Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika. Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Yesu, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. Akajitupa miguuni mwa Yesu akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria. Yesu akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” Yesu akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”