Luka 2:8-20
Luka 2:8-20 NEN
Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.” Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.” Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe. Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. Lakini Maria akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.