Luka 20:1-26
Luka 20:1-26 NENO
Siku moja, Isa alipokuwa akifundisha watu Hekaluni na kuhubiri Habari Njema, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati, pamoja na wazee wa watu wakamjia. Wakamuuliza, “Tuambie, unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Ni nani aliyekupa mamlaka haya?” Akawajibu, “Nami nitawauliza swali. Nijibuni: Je, ubatizo wa Yahya ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?” Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga mawe, kwa sababu wanaamini kwamba Yahya alikuwa nabii.” Basi wakajibu, “Hatujui ulikotoka.” Isa akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.” Akaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu. Wakati wa mavuno ulipofika, akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili wampe sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza. Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba. “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’ “Lakini wale wapangaji walipomwona, wakasemezana wao kwa wao. Wakasema, ‘Huyu ndiye mrithi. Basi na tumuue ili urithi uwe wetu.’ Kwa hiyo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua. “Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wapangaji hawa? Atakuja na kuwaua hao wapangaji, na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!” Lakini Isa akawakazia macho, akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa: “ ‘Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni’? Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.” Walimu wa Torati na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja, kwa sababu walifahamu kwamba amesema mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu. Kwa hiyo wakawa wanamchunguza na kutuma wapelelezi waliojifanya kuwa wenye haki. Walitaka kumtega kwa maneno yake, ili wampeane katika uwezo na mamlaka ya mtawala. Hivyo wale wapelelezi wakamuuliza, “Mwalimu, tunajua unasema na kufundisha yaliyo kweli wala humpendelei mtu, bali wafundisha njia ya Mungu katika kweli. Je, ni halali sisi kulipa kodi kwa Kaisari, au la?” Lakini Isa akatambua hila yao, akawaambia, “Nionesheni dinari. Je, sura hii na maandishi haya yaliyo juu yake ni vya nani?” Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.” Akawaambia, “Basi mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.” Wakashindwa kumkamata kwa yale aliyokuwa amesema hadharani. Nao wakashangazwa mno na majibu yake, wakanyamaza.