Luka 23:13-25
Luka 23:13-25 NENO
Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami sikupata msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. Wala Herode hakumpata na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachilia.” [ Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.] Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyu! Tufungulie Baraba!” (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.) Pilato, akitaka kumwachia Isa, akasema nao tena. Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!” Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.” Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu, wakidai kwamba Isa asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda. Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe. Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Isa mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.